JE, KILA MCHEZO KWA WATOTO NI SALAMA?



Na, Emakulata Msafiri

Kulikuwa na watoto wachangamfu sana waliopenda michezo. Kila jioni, baada ya masomo, walikusanyika uwanjani kucheza mpira, kukimbizana, na kupanda miti. Michezo hii iliwapa furaha kubwa na kuwaunganisha kama marafiki wa kweli.

Siku moja, kundi la watoto waliamua kucheza mchezo wa kurusha mawe. Walijificha nyuma ya vichaka na kurushiana mawe kwa furaha, wakiona ni burudani kubwa. Hawakujua kuwa mchezo huo ulikuwa na hatari. Ghafla, jiwe moja lilimpiga mtoto mmoja aitwaye Juma machoni, akapiga kelele kwa maumivu na kuanguka chini.

Watoto walipigwa na butwaa. Waliogopa na kujilaumu kwa kile kilichotokea. Wazazi wa Juma walikimbizwa eneo la tukio na kumpeleka hospitalini. Bahati mbaya, daktari alithibitisha kuwa jicho moja la Juma limeharibika na hataweza kuona tena kwa jicho hilo.

Tukio hilo liliwafanya watoto wa kijiji kufikiria kwa kina juu ya michezo yao. Wazazi na walimu waliwaelimisha kuhusu umuhimu wa kucheza michezo salama. Kuanzia siku hiyo, watoto waliepuka michezo hatari na wakajifunza kucheza kwa njia zinazohakikisha usalama wao.

Kumbuka tu,

Si kila mchezo ni salama, na ni muhimu kufikiria madhara yanayoweza kutokea kabla ya kushiriki katika michezo fulani.



emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments