JINI MFISHA WATU

 

Adeladius Makwega-Moshi Kilimanjaro.

Kijiji kimoja kilikuwa na watu wengi, huku wakiishi kwa pamoja kidugu, katika kijiji hiki cha Ujamaa walikuwa na wakulima na wafugaji wanyama wa kila aina, kilimo na huu ufugaji uliwasaidia mno wanakijiji hao kupata mboga na vyakula vya kila siku huku kubadilishana bidhaa hizo kulifanya maisha yao ya kila siku yasonge mbele na miili yao kuwa na afaya njema.

Kwa desturi ya mwanadamu amejawa na tamaa, wale waliofuga sana pia walitaka kuwa wakulima na hata mkulima kuutamani ufugaji. Kilimo mchanganyiko/ kilimo mseto ilikuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku. Matumizi ya wanyamakazi katika kilimo chao kama vile punda, farasi , ngamia na ng’ombe yalisaidia mno kuweza kupata mazao maradufu na kijiji hiki kuendelea mno, huku wakijenga nyumba bora zilizoezekwa kwa mabati mazuri za kila rangi yalitoka mbali mno na kufika hapa kijijini.

Tamaa ya kufunga na kulima ilikuwa uraibu wa kila mwanakijiji na hali hiyo kuwaambukiza hata wanavijiji wengine, Vijiji jirani navyo vikaingia moyo huu wa kijiji hiki kilichopata bahati ya kujua ufugaji na kilimo bora kutoka kwa wageni waliopita njia kwa kupotea na hilo kuwa ngekewa ya wanakijiji hawa nduguze Mwanakwetu.


 

Mkulima Bora wa Kilimo Mseto

Miongoni mwa wafugaji wa kijiji hiki alikuwa ni baba mmoja hodari, Mkomangi Bini Mkongeni ambaye alikuwa na ng’ombe, mbuzi , kondoo, farasi, punda, ngamia  na wanyama wadogo wadogo wengi wasiohesabika. Hapa Kijijini kama mtu alikuwa na sherehe kama vile jando , unyago na ndoa hodi za kila mara zilikuwa nyumbani kwa Mkomangi Bini Mkongeni na muitikio wa rabeeka kwa kila apigae hodi ilikuwa adaa ya ndugu huyu.

“Hodi Bini Mkongeni , mie ni Mbui Kalimang’asi nina harusi ya binti yangu kesho kukicha salama ndiyo hivyo napokea posa, naomba uniuzie fahari moja ili likachinjwe katika harusi ya binti yangu.”

Nyumbani hii ilipambwa na sauti ya milio ya wanyama hao zinazosikika huku zikiwa kama vile nyimbo za sherehe za jando na unyago. Maisha yalikuwa haya haya, ugeni wa mzee Kalimang’asi ulipokelewa na kukamatiwa fahari mmoja ambalo lilihasiwa vizuri ili nyama yake iwe kwa matumizi haya haya ya chakula na naye mzee Kalimang’asi  alilipa magunia 50 ya  karanga na kisha kuondoka zake. Mifugo ya Mkomangi Bini Mkongeni ilinawili mno na hivyo kuwa na maumbo ya ajabu na kutishia kijiji chote ,

“Bini Mkongeni analima na kufuga kwa kutumia dumba yaani uchawi , hizo ndumba kapata wapi?Na sie tukaununue?”

Suala hili likafikishwa kwa Mbui ambaye alikuwa ndiye chifu wa eneo hili,

“Kama kufuga tunafuga sote vizuri, iweje mifugo ya Bini Mkongeni iwe bora iwe inanawili kuliko yetu? Mbui tupe jawabu katika hili, tunafahamu mashamba yake yanapendeza, ngoko(gala) zake zimejaa vyakula, kwanini sisi sote hatuna hizo baraka ?”

Mbiu aliposikiliza shauri hilo aliwaambia kuwa amepokea malalamiko haya na kisha atayafanyia kazi. Mbui alifanya utafiti wa hilo na mwisho akwaita kikaoni kutoa majibu ,

“Jamani katika hili, kikubwa nawaombeni tujifunze kwa Bini Mkongeni, yeye siyo mgeni, yeye ni ndugu yetu , kwa namna anavyofanya kazi tunapaswa tu kumuiga na hilo tukifanya sisi sote tutakuwa na baraka na kijiji chetu kitasonga mbele.”

Majibu ya Mbui Mbeketu kwa wanakijiji hawa yalipokelewa lakini kwa shingo upande huku safari za kwenda kubadilishana mifugo na chakula zikiongezeka na nyumbani kwa huyu ndugu kuwa kama mnada mdogo. Kijijini watu wananufahika ama kweli baniani mbaya kiatu chake dawa na uhodari na ndugu huyu watu wamejawa na wivu na chuki, huku wakimnenea mabaya ndugu huyu.


 

Maneno yalivuma mithili ya kimbunga cha kiangazi, gafla kukaanza balaa la wanyama kupotea kidogo kidogo, walianza vifaranga vya kuku, kisha kuja kuku, wakaja bata, paka na mbwa. Mshangao ukawa unaongezeka, shida nini? Gafla wakaanza kupotea mbuzi kijiji kizima, mbuzi wote hawaonekani walipo. Upotevu ukatamalaki, wakafuata  kupotea kondoo baada mwezi mzima walipotea kondoo wote, milio ya kuku, mbwa, paka na hata mee ikawa adimu kijijini. punda , farasi nao ngamia wakapotea kama kimaajabu ajabu tu.

Ramli Mbele ya Mbui Mbeketu

Kijijini kikao kikaitishwa kujua shida ni nini, safari hadi kwa Mbui Mbeketu ili yeye awaongoze kuangalia katika kioo–kupiga ramli. Mbui Mbeketu akawaita wajuzi wa ramli kutoka huko Ungindoni na Upogoloni na kufika hapa kijijini na kupiga ramli yao hadharani uwanjani.

“Majibu ya ramli zote yakimuangikia Mkomangi Bini Mkongeni, balaa anafunga wanyama ambao wengine ni mwiko na haramu kufugwa hapo kijijini tangu enzi na jambo hili lisipofanyiwa kazi basi hatua kwa hatua kijiji chetu kitapotea bure.

Hoja ya pili ya majibu ya ramli ni kwa kuwa nyinyi wanakijiji mlikuwa mnanufahika sana na ufugaji wa Bini Mkongeni lakini hamkupaswa kumnenea mabaya ndugu wa damu moja. Mnyama anayekula mifugo sasa atakiangamiza kijiji na mnyama mwenyewe ni NUNDA wengine wakimuita  jini”

Mbui Mbeketu akatoa fatua kuwa sasa ni kumsaka tu huyu mnyama, kila mmoja arudi nyumbani kwake , kisha mrudi hapo kikao mkiwa na silaha huku akina mama wawapikie waume zao mabumunda ya ndizi mbivu za unga wa mahindi kuyatumia kama chakula vitani kumsaka Nunda/jinni. Wanakijiji sasa wanarudi nyumbani kuchukua silaha waanze vita vya kumsaka NUNDA walipofika katika visingiti vya milango yao wanashangaa hakuna mfugo hata mmoja majumbani,

“Astagafululai huyu JINI, filauni kabisa sasa katuachia nini hapa kijiji kama siyo umasikini?”

Mama Mjamzito AsalIa Kijijini

Kijiji kikapata taharuki ya pili, gafla wakaanza kuliwa watu, NUNDA akawagegedua vizuri wanakijiji wote tangu watoto, vijana , wanaume na kisha kumalizia wanawake. Kwa bahati nzuri nyumba kwa Bini Mkongeni alikuwepo mama mmoja, mke wake aliyekuwa anakaa ndani, kusubiri kujifungua wakati wa harakati hizo zinaendelea huyu mama alikimbilia katika pango moja na huko pangoni akajifungua mtoto wake wa kiume huku akiishi kwa kula mihogo mpira na mihogo michungu tu iliyokuwa kando ya pori hilo.

Mtoto huyu aliyezaliwa alikuwa wa ajabu, katika kila siku aliyokuwa anaishi ilikuwa sawa na miaka 10, hivyo ndani ya siku mbiIi alikuwa na umbo sawa na kijana mwenye miaka 20 huku akimuuliza mama yake mbona anaishi mwenyewe? Majibu yalikuwa kama kama kilivyo kisa hiki cha NUNDA hapo kijijini na hata baba yake mzazi Mkomangi Mkongeni kaliwa na NUNDA, kijana huyu alipata ghadhabu kubwa. Nunda alikuwa na uwezo wa kujua kuwa yupo mtu mmoja hajammeza huku akimsaka na hapo sasa Nunda akawa anakula majani tu.

Nunda anafanya msako huku na kule naye mama wa watu na kijana wake wako pangoni. Kijana huyu aliposimuliwa kisa chote hiki akatoka zake usiku mmoja na kuongozwa na mama yake kwenda katika eneo ambalo lilikuwa makazi yao, mandhari ya eneo hilo kulikuwa na vyombo kadhaa vipo nje kama vinu, majiko vyakula vimeanikwa lakini hakuna watu, hali ni ukimya tu wakisikika wadudu wanalia kwa mbali. 


 

Kaguakagua humo ndani kumbe baba yake mzazi huyu kijana alikuwa na bunduki, kijana akaichukua ile bunduki iliyokuwa na risasi tatu na kukata shauri kwenda kumsaka JINI MLA WATU. Mama wa huyu kijana alimuomba mwanawe kwanza warudi pangoni ili akampe kitu, kweli walifanya hivyo kwa sababu moja kubwa ili mama mtu abaki eneo salama, hapo alipofika alimpatia mwanae vipande vitatu vya mihogo michungu ambayo alitakuwa kula kipande kimoja kwa siku moja na kuanza vita vya kumsaka huyu JINI, mama akibaki pangoni.

Kumbuka JINI anayo hisia, anashangaa mbona huku kijiji kunamtu mwingine mbona simuoni? Jini akiwa na mashaka ya usalama wake, Jini akaongeza hasira na kwenda kuwasaka hao watu. Msako wa kusakana pande zote ukaanza, saka saka na wewe.

Siku ya kwanza majira ya jioni akazunguka hadi upande wa mwisho wakijiji akakutana na mnyama mmoja akampiga risasi kisha akaanza kuimba.

“Mama njoo ulole Jini Mla Watu, Mama Njoo Ulole Jini Mla watu.”

Mama yake akawa anajibu akiwa pangoni, maana sauti za mawasiliano zilikuwa zinafanyika kimiujiza.

“Mwanangu huyo siyo Jini Mla watu Mwanangu huyu siyo Jini Mla watu.”

Kijana akaendelea na kupambana na siku pili majira ya jioni akasikia kimbunga kimoja kikubwa kweli, kijana kwa uwoga akafyatua bunduki yake katika kimbunga hiki kumbe ulikuwa upepo tu maana eneo hilo lilikuwa tupu , kuja kutahamaki hakuna kitu. Siku ya tatu kijana yu msituni ana risasi moja na kipande kimoja ya muhogo mchungu,muhono mchungu anakula huku ukimuondolea uisingizi, mara akisikia sauti ya radi na ngurumu tele na kaiha mvua kubwa kunyesha, mara ukatokea uvumi na upepo mkali huku miti ikiwa inadondoka chini, mara kijana huyu akaliona jitu kubwa linalotisha likimfuata kwa kwa hasira zote, lina ulimi mrefu, meno yake nje, lilikuwa na taswira zote na maumbile ya kike lakini tabia za kiume linamkaribia, udenda ukimtoka huku jitu hili likiwa na macho makubwa na sasa likakaribia kumkamata kijana huyu masikini wa watu. Macho ya jitu hili yalikuwa yanadanganya ukarimu wa kiumbe, macho yalikuwa  hatari mno. Kijana huyu akafyatua bunduki yake na kulipiga jichoni hili dudu na dudu hili kufa hapo hapo.

“Mama njoo ulole JINI Mla watu Mama njoo ulole Jini mla watu”

Mama wa huyu kijana akajibu kwa Kuimba,

“Mwanangu huyu ndiyo Jini Mla watu Mwanagu huyo ndiyo Jini  mla watu.”

Kweli mama huyu alitoka pangoni hadi alipo yule kijana na Nunda aliyekufa akiwa kando, mama huyu akampongeza kijana wake kwa kazi nzuri na kusema kuwa hapa kazi bado anachotakiwa kufanya achukue kisu kipya kisha akata tumbo la huyu Nunda, Nunda Mla Watu. Kijana alifuata maelekezo ya mama yake na kufuuta chuma na kukifua vizuri kisha kurudi alipo Nunda kumkata tumbo gafla alipomkata tumbo mnyama huya walitoka wanyama wote walioliwa na huyu Nunda tangu mdogo hadi mkubwa na kisha kutoka wanakijiji wote wakiwa hai wanashangilia wakisema

“Mwanakwetu Umetukomboa.”

Mtu mwisho kutoka alikuwa Mbui Mbeketu ambaye aliwaomba wanakijiji hawa wakae chini Yeye na Mkomangi Bini Mkongeni, mama wa huyu kijana wao na huyu kijana wapande juu ya nyama ya Nunda na kisha Chifu Mbeketu kutoa maelezo haya.

“Jamani Mwanakwetu amekutomboa, hivo tumepewa wasaa wa kurudi tena kijijini tunapaswa kuishi kwa kubadilika tabia yale mambo ya kale tuachane nayo , nani anataka kurudi katika tumbo la NUNDA? Kila mmoja akate kipande cha Nunda aende nacho kwake akile na ndiyo kiwe chakula cha kwanza kula kuonesha kuwa shughuli sasa imekwisha na Leo hii mie Mbui Mbeketu nauvua Umbui nakumpa huyu Kijana awe kiongozi wetu kuanzia leo.”

Watu wanatoka na vipande vya nyama na kurudi majumbani mwao, kila mmoja ile anafika kwake anashangaa mifugo yake imerudi nyumbania kwake kama ilivyokuwa awali naye kijana kurudi kwa wazazi wake huku wakikuta rundo ya mifugo na mazao kama mwanzo na kijijini waliishi vizuri chini ya uongozi wao mpya.


 

Mwanakwetu upo ?

Mkumbuke

“Nunda Mfisha Watu.”

Nakutakia Siku Njema

makwadeladius@gmail.com

0717649257



















 

0/Post a Comment/Comments