
Adeladius Makwega-Moshi KILIMANJARO
Katika sebule ya nyumba hii nilikutana na picha kadhaa, vitabu. Makabati, vyombo na karatasi za michoro ya sehemu za mwili wa binadamu , huku kukiwa na kalenda moja tu ya mwaka wa 2025.
Macho yangu niliyakodoa kodoo na nilipoitazama vizuri kalenda hii iliyotundikwa juu umbali ya mita tatu kwa macho yangu ya uzee uzee, hapa nilikuwa sioni vizuri, hivyo niliomba ruhusa kwa wenye nyumba hii waniruhusu niitungue Kalenda hii kutoka angani kisha niione kwa karibu.
Msomaji wangu tambue kuwa macho ya mtu mzima kuwa na hitilafu kuona ni jambo la kawaida maana macho ya mtu mzima yameona vingi hapa duniani, lakini kumbuka tu msomaji wangu Bibilia imetaja neno macho mara nyingi ikisisitiza haya;
“Jicho lako ni nuru ya mwili wako, Usiruhusu jicho lako lione mambo yasiyofaa na Macho yako yaliniona tangu sijazaliwa.”
Kwa wale wasomaji wenye umri mdogo wanaweza kuona kuwa, aaah Mwanakwetu hali mboga za majani, Mwanakwetu hali chakula bora, Shabashi! Mwanakwetu ale mboga za majani kwani yeye mbuzi ! Ahh lakini nisikupwage msomaji wangu, mie nakula mboga za majani mno na nakula kama meee(Mbuzi).
Tatizo la macho ya Mwanakwetu ni uzee tu na anatakiwa kuvaa miwani lakini sasa Mwanakwetu akivaa miwani anachekesha sana anakuwa kama Jeel White wa Family Matters.
Kumbuka msomaji wangu Kalenda imeshatunguliwa kutoka ukutani mwa nyumba hii, kwa kuikodolea tu kwa karibu Mwanakwetu aliona haya;
“Mwezi machi wa 2025 una siku 31 , kukiwa na sikukuu ya Eid el Fitri kama mwezi utaandama tarehe za Machi , 2025. Pia Mwezi Aprili 2025 kama mwezi utaandama mwezi wa nne lakini mwezi wa nne una sikukuu kubwa nyingi ; Karume Day, Ijumaa Kuu, Pasaka, Jumatatu ya Pasaka na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.”
Juu ya tarehe za miezi hii miwili yaani siku 61 kulikuwa na picha tatu; ya juu wanafunzi kama wanafanya mitihani, ya pili wanafunzi wa madarasa nadhani chekechea wanasoma na picha ya tatu wnafunzi wa darsa kama la kwanza au la pili wanasoma. Nilivutiwa sana na kalenda hii ,huku nikiisanifu kurasa moja baada nyingine, kukiwa na picha kadhaa tangu kurasa ya kwanza hadi ya saba. Nilikutana na picha nzuri za mazingira ya shule, picha za walimu, watawa wa Kanisa Katoliki wakiwa na vilemba vyao kichwani.
“Nikakumbuka nilipokuwa mdogo, watoto wenzangu walikuwa wananiambia masista huwa hawavui vilemba vyao, nikiwa mdogo nikawa najiuliza je hawa masista nywele zao wanasuka, wanachana au wanaweka dawa?, Jibu sikulipata.”
Picha zingine zilionesha wanafunzi wakiwa wamevalia sare za michezo huku walimu wakiwa kando yao.
Hayo yote yalifanya Mwanakwetu kuuliza swali juu ya kalenda hii,
“Hii Kalenda ni ya shule ya Msingi ya Mtakatifu Katarina Lushoto Mjini inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga. Mimi nasoma hapa mzee, tuliambiwa tulipe shilingi 5000/= na kila mwanafunzi na aliyelipa alipewa kalenda hiii.”
Kwa hakika niliipenda Kalenda hii ya shule ya Mtakatifu Katalina hapa Lushoto Mkoani niliyoikuta imebandikwa katika nyumba hii ambayo ilinishawishi niitungue kutoka angani.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa haki nilijifunza umuhimu wa taasisi yoyote kuwa na kalenda yake kwa mwaka husika, kwa hakika kwa taasisi kama shule kalenda pia inaweza kusaidia kuwa chanzo cha kuingozea mapato taasisi hiyo lakini pia inasaidia pia kwa shule husika kujulikana kwa watu wengine.
Jambo hili linaweza kufanya si kwa shule tu, bali hata Kanisa, Msikiti na taasisi zingine kutengeneza kalenda zao kisha kuwauziwa wanajumiya hiyo na wakati mwingine kunaweza kutengeneza kalenda za matukio yenu na kuzigawa bure huku shughuli mnazofanya za maendeleo ya jamii zinafahamika.
Mwanakwetu Upo?
Kumbuka
“Kalenda Iliyotunguliwa Angani.”
Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment