KISOGO CHANGU KIKOJE



 

Adeladius Makwega Moshi Kilimanjaro

 

Jamii za kiafrika zina mambo mengi ambayo hufundisha kwa namna tofauti tofauti, mojawapo ya elimu katika jamii zetu huwa mara baada ya mama kujifungua tu huwa anapewa maelekezo ya namna ya kumlaza mtoto mchanga.

 

“Mwanakwetu angalia mtoto wako usimlaze upande mmoja, mlaze kwa kumgeuza geuza hili kisogo chake kikae vizuri.”

 

Hilo ni mojawapo ya maagizo ambayo akina mama wanaojaliwa kujifungua hupewa ikiaminika kuwa pengine kama mtoto akilazwa vibaya basi kisogo/kichogo chake kinaweza kuwa paba(Wazaramo wanaita Batebate), kinaweza kuwa kimechongoka sana kuwa na umbo kama kisu, kisogo cha duara au hata kisogo chenye chemba/chogo chemba-kisogo chenye uwazi.

 

Waswahili tunaamini yote hayo majina ya visogo yanatokana na namna mtoto anavyozaliwa au atakavyolazwa, narudia kusema kwa mujibu imani nyingi za kiafrika.

 

Msomaji wangu ebu nikupe kazi kidogo ya kutazama mtu yoyote aliye jirani yako hapo ulipo iwe kushoto, kulia, nyuma au mbele yako, je kisogo chake ni cha umbo gani?

 

Nina hakika sasa majibu yataangukia katika batebate/bapa, chogo chemba, chogo cha kisu au kisogo cha duara.

 

Sina hakika kama jambo hili ni la kweli kisayansi lakini hiyo ndiyo imani ya makabila mengi ya kiafrika tangu enzi kwa kuwa umbo la kichwa cha mtoto huwa linatengenezwa na mama au mlezi anayemtunza mtoto baada ya kuzaliwa.

 

Ndiyo kusema kichogo cha mtoto kikiwa na umbo fulani kati hayo ya niliyotaja wa kupongezwa au kulalamikiwa ni mama /mlezi wa mtoto huyo wakati akiwa mchanga. Lawama hii mara zote ni abadani baba kubebeshwa mzigo huo.

 

“Mama akigoma kubeba lawama hizi anajidanganya basi asizae watoto na aache kulea hao watoto anaowaza kama hilio linawezekana.”

 

Msomaji wangu umbo la kisogo liwe baya au zuri mwenye kisogo hicho ni adimu kujua labda kwa kujitazama katika kioo au kuambiwa. Kwa mazingira ya pwani huwa watoto wadogo hutumia sifa hizo za kisogo na maumbile mengine kuwalaani wenzao.

 

“Ondoka hapa na kisogo chako chemba, Ondoka hapa na kisogo chako cha batebate (bapa). Nenda zako na kisogo chake kilichochongoka kama kisu kisije kutuchoma.”

 

Ukiyasikia maneno hayo utabaini kuwa ahaaa kumbe kisogo changu kiko cha namna hiii. Unapoambiwa maneno hayo mara zote huwa inaumiza sana lakini ndivyo ulivyo na huo ndiyo ukweli.

Kwa kuwa kisogo ni maumbile tu hauwezi kuyabadilisha lakini unapoambiwa na namna unavyojibu ina maana kubwa sana kwako na wale wanaokulaani.

 

“Ahaaa mnanicheka kisogo changu sawa ngojeni na nyie mzae wa kwenu tuwaone. Kweli kisogo changu kipo kama kisu, sogea karibu kikuchome.”

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

 

Hapo Mwanakwetu yale madhaifu yanayotajwa yanakuwa darasa kwa wengine na jamii nzima.Hii inasaidia kuondoa ugomvi kwa yule anayeambiwa na yule anayetaniwa na kujenga udugu.

 

“Ahaa yule hana neno hakasiliki kila tunavyomwambia.”

 

Hii inajenga udugu wa karibu baina yao na jamii na jamii.

 

Mwanakwetu kumbuka kuwa mtoto hulazwa na kugeuzwa geuzwa siyo kumlaza upande mmoja tu.Mwanakawetu leo nisiyaseme mengi naomba niishie hapo kwa kukuuliza swali moja tu je mwenzetu unatambua kichogo chako kikoje, Je batebate/paba, kama kisu, chogo chemba au duara? 


 

Mwanakwetu upo

Kumbuka

“Kisogo Changu KIKOJE.”

Nakutakia siku Njema.

 

makwadeladius @gmail.com

 

0717649257 








 

0/Post a Comment/Comments