Na, Emakulata Msafiri
Kulikuwa na watoto waliopenda kucheza kila jioni baada ya kutoka shuleni. Mchezo walioupenda zaidi ulikuwa Kombolela, ambao uliwafanya wakimbie, wajifiche, na kushirikiana kwa umoja.
Siku moja, kundi la watoto likiongozwa na Amani na Zawadi lilikusanyika uwanjani kama kawaida. Amani alikuwa hodari wa kujificha, wakati Zawadi alipenda kumkomboa kila mtu haraka. Mchezo ulianza kwa Juma kuwa mtafutaji, na wengine wote wakatawanyika kutafuta sehemu nzuri za kujificha.
Amani alijificha nyuma ya shina kubwa la mti wa mwembe, huku Zawadi akiteleza chini ya kichaka. Juma alianza kutafuta, akitazama kila kona kwa makini. Mara akamuona Juma mdogo akijificha nyuma ya gunia na kwa haraka akamgusa, akisema kwa sauti, "Gwaride!"
Wengine walibaki kimya, wakitumai kuwa hawatagunduliwa. Lakini ghafla, Zawadi aliona nafasi, Juma alipokuwa akimtafuta mwingine, akakimbia kwa kasi hadi eneo la kombolela na kugusa, akisema kwa sauti, "Kombolela!" Watoto waliokuwa wametekwa walishangilia, wakirudi kwenye mchezo.
Mchezo uliendelea kwa furaha, kila mtoto akijitahidi kujificha vyema au kukimbia kwa kasi ili kumkomboa mwenzake. Jioni ilipofika, wazazi wakawaita watoto warudi nyumbani, lakini walikubaliana kuwa kesho watakutana tena kuendeleza mchezo wa kombolela, ambao uliwafanya waungane kama marafiki wa kweli.
Mchezo huu haukuwa tu wa kujifurahisha, bali pia uliwafundisha mshikamano, ujanja, na umuhimu wa kusaidiana. Na hivyo, kila siku, watoto wa kijiji walibaki na kumbukumbu nzuri za kombolela, mchezo uliowajenga kuwa jasiri na wenye upendo.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872
Post a Comment